Alhamisi 4 Juni 2026 - 11:51
Marji' na Mwanazuoni Mkubwa wa Najafu Afariki Dunia

Hawza/ Dunia imepata mshtuko wa ghafla baada ya Madrasa ya Ahlulbayt (as) kuondokewa na Mwanazuoni mkubwa katika zama hizi, Marji' mkubwa Ayatullah Muhammad Is-ha'q Fayyadhi (ra)

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu na hakika Kwake Yeye tutarejea... Kwa masikitiko na huzuni nyingi, tunatoa rambirambi kwa Sahib al-Asr na Waliyy al-Amr, Mwenyezi Mungu aharakishe faraja yake, kwa vyuo vya elimu ya dini, kwa Waislamu wote kwa ujumla, na hasa kwa wafuasi na familia ya marehemu; tunamuomboleza Marji', faqihi, mwanazuoni wa usuli, na mmoja wa mujitahidi mashuhuri zaidi wa zama hizi katika elimu ya Rijal al-Hadith, Sheikh Muhammad Ishaq al-Fayyadh, mwenye asili ya Afghanistan na mkazi wa Najaf; ambaye amefariki dunia baada ya kuugua, akiwa ameacha urithi mkubwa wa tafiti na masomo ya kielimu, hasa katika elimu za fiqhi, usuli na Rijal al-Hadith, ambazo alizitumia kuzinufaisha duru za masomo na utafiti katika Hawza kubwa ya Najaf Ashraf na hawza nyingine za Kishia.

Naye ndiye aliyepata umaarufu kupitia taqrirati zake za elimu ya usuli za mwalimu wake Sayyid al-Khoei — Mwenyezi Mungu aitie manukato kaburi lake — zinazojulikana kwa jina la Muhadharat al-Fayyadh, ambazo wanafunzi wa Bahth al-Kharij bado wanaendelea kunufaika nazo kwa takribani nusu karne.

Darsa zake zilihudhuriwa na wanafunzi wa hawza wenye ubora wa kielimu, vilevile vitabu vyake bado ni chemchemi kwa wanafunzi wa ijtihadi na faqaha, hususan: "Mabahith za al-Rijali" na "Mabahith za Usuli".

Alijitofautisha kwa nguvu ya utafiti wake katika elimu ya usuli; kwa sababu hiyo wanafunzi waliokuwa wakifuatilia darsa zake za usuli walikuwa wengi zaidi kwa kiasi fulani, kwa kuwa alikuwa miongoni mwa wale walioamini kuwa A'lamiyyah hupatikana kwa yule ambaye ni mwenye elimu kubwa zaidi katika elimu ya usuli na misingi yake, na hili ni suala la hitilafu baina ya mafaqihi. Mwenyezi Mungu amlipe mema na kwa Mwenyezi Mungu ndio malipo yake.

Vyuo vya elimu ya dini vitamkosa, lakini ataendelea kuwa hai kupitia wanafunzi wake na athari zake, kwa kuondoka kwake, Najaf Ashraf inapoteza nguzo mojawapo ya Marjaiyyah yake. Mwenyezi Mungu awarefushie umri waliobaki, hasa Marjaiyyah ya juu, kwa haki ya Muhammad na kizazi chake kitoharifu — sala na salamu za Mwenyezi Mungu ziwe juu yao wote.

Shirika la Habari la Hawza, linatoa mkono wa pole katika siku ya Ghadir kwa familia yake, jamaa zake, na Mashia wote wa Bwana wa wachamungu na Amir al-Mu'minin — Mwenyezi Mungu aturuzuku kumzuru na kuwa jirani naye katika maisha na baada ya kifo — hakika Yeye ni Mwenye kusikia na Mwenye kujibu dua.

Na kwa roho yake na roho za waumini wanaume na wanawake waliotangulia, thawabu ya Suratul-Fatiha.

18 Dhul-Hijjah 1447/ June 4 2026

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha